Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) imepokea ndege ya Shirika la Air Cairo kutoka Hurghada, nchini Misri, ikiwa na abiria 59, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), majira ya saa 12:10 asubuhi ya leo Jumapili ya tarehe 01 Novemba 2026.

Ndege aina ya Airbus A320 inatarajiwa kuhudumia safari za Zanzibar mara nne kwa wiki ambapo leo iliondoka katika Uwanja huo ikiwa imebeba jumla ya abiria 73.

Kuanzishwa kwa safari hizi kunatarajiwa kuimarisha muunganiko wa Zanzibar na soko la utalii la Misri, kuongeza idadi ya wageni na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.

Katika mwaka 2026 hadi sasa jumla ya mashirika manne mapya ya ndege ya kimataifa yameanza safari zake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), yakiwemo Bul Air, Airlink, EgyptAir na Air Cairo. Aidha, Shirika la Ndege la British Airways limetangaza rasmi kuanza safari zake za kuunganisha jiji la London na Zanzibar ifikapo tarehe 29 Mei 2027, mara tatu kwa wiki.

Juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha miundombinu na kukuza sekta ya utalii zinaendelea kufungua fursa mpya za uwekezaji na kuongeza muunganiko wa Zanzibar na mataifa mbalimbali kupitia usafiri wa anga.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar itaendelea kuimarisha huduma na kuboresha mazingira ya kiutendaji ili kuvutia mashirika mapya ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari zake za moja kwa moja (direct flight) kuja Zanzibar, hatua itakayochangia kuongeza muunganiko wa Zanzibar na mataifa mbalimbali pamoja na kukuza sekta ya anga na utalii