BODI YA WAKURUGENZI ZAA YATEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO AAKIA.

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Ndugu Juma Burhan, leo Jumamosi, Agosti 22, 2026, imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA).

Katika ziara hiyo, Bodi imetembelea mradi wa ujenzi wa Jengo jipya la Abiria la Terminal 2, ambalo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 1,400,000 kwa mwaka. Mradi huo, wenye gharama ya takribani Dola za Marekani milioni 34, umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2026.

Bodi pia imekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa maegesho mapya ya ndege (New Apron), unaolenga kuongeza uwezo wa AAKIA kuhudumia ongezeko la ndege na abiria, sambamba na kuboresha usalama, ufanisi wa shughuli za ardhini na huduma za usafiri wa anga. Mradi huo umefikia asilimia 25 na unatarajiwa kukamilika Agosti 1, 2028.

Baada ya ziara hiyo, wajumbe wa Bodi wamepokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali inayosimamiwa na Mamlaka, ikiwemo mradi wa Daraja la Kuunganisha Terminal 2 na Terminal 3 (Link Bridge) ambao umefikia asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika Desemba 15, 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Ndugu Seif Abdalla Juma amewaeleza wajumbe wa bodi kuhusu miradi ambayo tayari imekamilika kwa asilimia 100, ikiwemo ukarabati wa Jengo la Terminal 1 kwa ajili ya kuhudumia viongozi wakuu wa nchi, wageni mashuhuri na huduma za ndege binafsi, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Biashara katika Terminal 3.

Ziara hiyo imeiwezesha Bodi ya Wakurugenzi kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kupokea taarifa ya hatua zilizofikiwa, ikiwa ni sehemu ya jukumu lake la kusimamia maendeleo na utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar.

Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendelea kuboresha na kupanua miundombinu ya viwanja vya ndege, ili kuongeza uwezo wa kuhudumia idadi inayoongezeka ya abiria na ndege na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika sekta ya usafiri wa anga.