MAKAMU WA PILI WA RAIS AIPONGEZA ZAA KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO AAKIA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, jana amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Biashara (Business Centre) na ukamilishaji wa Jengo la Pili la Abiria (Terminal 2).

Katika ziara hiyo, Mhe. Hemed aliambatana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, ambapo walipata maelezo kutoka kwa viongozi na wataalamu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kuhusu maendeleo ya miradi hiyo na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake.

Amesema miradi hiyo ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia sekta za usafiri wa anga, utalii na biashara, huku akiwasisitiza kuendelea kuhakikisha kazi zote zinakamilika kwa ubora wa hali ya juu na kwa kuzingatia muda uliopangwa.

Makamu wa Pili wa Rais pia amesisitiza kuwa maandalizi ya miundombinu ya kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume yana umuhimu mkubwa kuelekea mashindano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda itakuwa mwenyeji wake.

Amesema Zanzibar inatarajia kupokea wageni wengi, wakiwemo timu, viongozi, wawekezaji na mashabiki wa soka kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni lazima miundombinu ya viwanja vya ndege iwe katika viwango vya kimataifa ili kutoa huduma bora na kuendelea kuitangaza Zanzibar kama lango la utalii na uwekezaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, amesema Serikali itaendelea kutoa usimamizi wa karibu katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kukidhi viwango vinavyotakiwa, sambamba na kuimarisha uwezo wa uwanja huo kuhudumia ongezeko la abiria na shughuli za kiuchumi.

Miradi ya Kituo cha Biashara (Business Centre) na Jengo la Pili la Abiria (Terminal 2) ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga ili kwenda sambamba na viwango vya kimataifa.